Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yaingiwa na hofu kwa kiwango bora wanachoonyesha timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) katika
Mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup yanayoendelea nchini Kenya.
Hofu hiyo imekuja jioni ya leo katika uwanja wa Kenyatta Mjini Machakos mara baada ya kutoka sare ya 0-0 na Wenyeji Kenya na kupelekea Zanzibar kutinga moja kwa moja nusu fainali wakiwa na alama 7 wakiongoza kundi lao A lenye Mataifa kama Kenya, Libya, Rwanda na kaka zao Tanzania bara.
Baadhi ya wajumbe wa CECAFA wakiongozana na wakaguzi wanaopinga dawa za kuongeza nguvu Michezoni walikwenda kwenye vyumba vya kubadilisha nguo vya Zanzibar Heroes kwa kusema haiwezekani timu ya Zanzibar icheze michezo mitatu mfululizo bila ya kuonekana kuchoka.
“Mechi tatu mfululizo Zanzibar wanacheza kwa kiwango bora, tena wachezaji wao ndo wale wale kila siku wanaoanza labda abadilike mmoja tu, itakuwa wanatumia dawa za kuongeza nguvu lazima wachunguzwe”. Alisema mmoja wa Afisa.
Uongozi wa Zanzibar Heroes ukakubali wachezaji wake kwenda kupimwa kama kweli wanatumia dawa za kuongeza nguvu au kiwango chao tu,ukatokea mtafaruku baina yao wenyewe viongozi wa CECAFA na mwisho wakakubali kuwaachia wachezaji hao waende zao wachezaji ambao walishangazwa mno kusikia kuwa wanatumia dawa.