NI timu tatu pekee za Ligi Kuu Bara ambazo hazijapoteza hata mchezo mmoja hadi ligi hiyo inafikia katika mechi 10 kwa kila timu.
Vinara Simba ambao
wanaongoza wakiwa na pointi 22, Azam FC wanafuatia wakiwa na pointi hizo na mabingwa watetezi, Yanga, wenye pointi 20 katika nafasi ya tatu.
Katika timu ambazo hazijapoteza mchezo Azam FC inawezekana kabisa haikuwa imepewa nafasi ya kuwa ilipo sasa kutokana na kuamua kufanya mabadiliko makubwa.
Mabadiliko hayo yameonyesha kushangaza wadau wengi lakini haikuishia hapo tu, kwani hata wahusika pia wameonekana kushangazwa na kikosi chao.
Azam FC walitangaza malengo ya kukijenga kikosi chao upya, huku wakiwaachia nyota kadhaa waondoke, akiwemo nahodha John Raphael Bocco.
Mwendo wa kikosi hicho, umeufanya uongozi wa Azam FC kubadili mawazo na kutangaza sasa wanawania ubingwa na wala si walivyosema awali kwamba wanakijenga kikosi chao upya.
Huenda ilikuwa ni kauli ya kuanzia au kujihami kwa hofu ya mabadiliko waliyoyafanya. Kwamba walipanga kufanya jambo jema lakini hawakuwa na uhakika kama mambo yatakwenda vizuri haraka na sasa inaonekana kama wamekuwa “wanamkimbiza mwizi” kimyakimya. Na sasa hawataki utani hata kidogo.
Kupunguza wachezaji wakongwe huenda Azam FC kumewasaidia kuondoa presha lakini kutoa kauli kuwa wameanza kujenga kikosi kumewasaidia wachezaji wao kucheza katika kiwango kilicho bora zaidi.
Wachezaji wa Azam FC wamekuwa hawana ile presha kubwa na wameweza kucheza katika kiwango chao na ukiangalia wageni wengi wamefanya vizuri pia kwa kuwa wamefika sehemu ambayo imeonyesha haina presha kubwa.
Kweli, si kuwa Azam FC ilimuacha kila mchezaji muhimu. Angalia akina Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Aggrey Morris, Yakubu Mohamed, Bruce Kangwa, David Mwantika, Frank Domayo na wengine ni wachezaji wenye uzoefu na wana msaada.
Lakini ongezeko ndilo lilikuwa la vijana wengi. Huenda kuondoka kwa watu kama akina Bocco, Aishi Manula, Erasto Nyoni waliohamia Simba na Gadiel Michael aliyetua Yanga ilionekana kuwa kikosi kimesambaratika. Lakini ukitupa jicho makini utagundua kweli wachezaji muhimu waliondoka na wengi muhimu wamebaki.
Angalia Azam FC inakwenda ikiwa imecheza mechi kumi, kati ya hizo imeshinda sita, nne zikiwa nyumbani na mbili ugenini. Halafu ikachukua sare nne na kuifanya kuwa na pointi 22 bila kupoteza hata mechi moja.
Kwa mechi nne mfululizo zilizopita, Azam FC haijaruhusu lango lake kuguswa na timu yoyote na sasa baada ya mechi 10 za Ligi Kuu Bara, Azam FC ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache zaidi ya kufungwa (mawili tu). Si vibaya kusema kwamba Azam FC, ndiyo timu yenye safu bora zaidi ya ulinzi katika kipindi hiki.
Ambacho kinaonekana ni kuwa, ufungaji wao si mzuri sana kwa kuwa ina mabao nane ya kufunga na kwa sehemu waliyofikia kama wataanza kufunga mabao mengi, itakuwa presha kuu kwa Simba na Yanga ambao ndiyo wapinzani wao wakubwa.
Azam FC inaweza kwenda kwa mwendo huu au inaweza kuteleza pia kama wachezaji au viongozi watajisahau na kuona wameweza kila kitu.
Mwisho nisisitize kuwa kupitia Azam FC, kuna jambo la kujifunza. Kwa yeyote aliyechukua uamuzi ambao ulionekana mgumu, amesaidia kuleta mambo lakini waliosaidiana naye kufanya jambo liende, pia wanastahili pongezi.
Hakuna hofu ya kujifunza mwenzako anapofanya vizuri, sasa Azam FC wamefanya jambo ambalo linaweza kuwa somo kwa kila upande, basi litumieni hata kwa “kunyofoa” kidogo kuangalia mnaweza kupata kipi kizuri.
MECHI ZA AZAM FC:
.Ndanda 0-1 Azam
Yahaya Mohammed 34
Azam 0-0 Simba
Azam 1-0 Kagera
Mbaraka Yusuph 44
Azam 1-0 Lipuli
Mbaraka Yusuph 12
Singida 1-1 Azam
Danny Usengimana 39 Paul Peter 89
Mwadui 1-1 Azam
Hussein Kabunda Himid Mao 9 (penalti)
Mbao 0-0 Azam
Azam 1-0 Mbeya
Mbaraka Yusuph 59
Azam 1-0 Ruvu Azam
Yahaya Zayb 90+3