FAMILIA YAMWAGA UBUYU KUHUSU DEREVA WA TUNDU LISU - MAINFO93

Latest

Kuwa updated kwa kutembelea mainfo93, hapa utakutana na mastory toka kila kona ya ulimwengu wa dot com. Contact habarimtandaoni@gmail.com

Random posts

September 18, 2017

FAMILIA YAMWAGA UBUYU KUHUSU DEREVA WA TUNDU LISU

Familia ya Tundu Lissu.
IKIWA ni siku 10 baada ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi, familia yake imezungumzia tukio hilo na namna inavyomfahamu dereva wake kwa zaidi ya miaka 20.
Tangu kutokea kwa tukio hilo mchana wa Septemba 7 huko
Dodoma , dereva wa mbunge huyo, Simon Mohamed Bakari amekuwa akitajwa kama mtu muhimu anayeweza kusimulia tukio hilo na hata kusaidia kuwabaini wahalifu.
Hata polisi imekuwa ikimtaka ili imhoji ikisema ni shahidi muhimu katika tukio hilo. Hata hivyo, kijana huyo yupo
Nairobi akimuuguza bosi huku mjadala juu yake ukiendelea nchini.
Katika mahojiano na Mwananchi , familia ya mbunge huyo imeonyesha kuwa na imani kubwa na dereva hiyo ikibainisha inavyomfahamu kwa miongo miwili.

Akizungumza katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwa baba wa mbunge huyo, Lissu Mughwai katika Kijiji cha Mahambe, Kata ya Unyahati wilayani Ikungi, Singida, Muro Lissu ambaye ni kaka yake alisema hawana wasiwasi na dereva huyo kwa kuwa ni kijana aliyelelewa na mwanasheria huyo mkuu wa Chadema tangu akiwa na umri wa miaka 15.
“Yule kijana alienda kwa Lissu akiwa mdogo kama kijana wa kazi za nyumbani. Alimchukua katika Kijiji cha Sefuka kilichopo Magharibi mwa Singida . Tangu wakati huo alimfunza kazi zote akiwa pale nyumbani kwake. Amemlea, amekulia kwake,” alisema Muro.
Alisema dereva huyo alifundishwa mambo mengi akiwa mmoja wa wana familia ikiwamo kupelekwa kujifunza udereva. Muro alisema Lissu alipoanza harakati za kuwania ubunge mwaka 2007 alikuwa na kijana huyo.

Freeman Mbowe akiwa na dereva wa Lissu siku ya tukio.
“Amekuwa dereva wake tangu alipoanza kuhangaikia jimbo mpaka amechukua ubunge mwaka 2010 akawania tena 2015. Wana miaka mingi na yule kijana zaidi ya miaka 20 amemlea,” alisema Muro.
Alisema licha ya Lissu kutozungumza chochote kuhusu vitisho alivyokuwa akipewa na kufuatiliwa na watu wasiojulikana, dereva wake alikuwa akiitaarifu familia kuhusu matukio hayo kila yalipotokea, hivyo walijua kinachoendelea kupitia kwake.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Ikungi, Jihala Ibrahim
aliyekuwapo pamoja na wanafamilia katika mahojiano hayo alisema licha ya kuchanganyikiwa, dereva huyoalielezea tukio zima lilivyokuwa baada ya wao kuwasili hospitalini Dodoma wakitokea Ikungi.
“Nilikutana na dereva wake Dodoma baada ya tukio, kwa kweli yule kijana alikuwa amechanganyikiwa na mpaka anaondoka siku ya pili kwenda Nairobi alikuwa ameathirika kisaikolojia,” alisema.
Ibrahim anaamini kuwa kama asingekuwa dereva huyo, Lissu asingepona kirahisi, “Dereva wake anasema tangu wanatoka bungeni, magari mawili yalikuwa yakiwafuatilia na kila alipojaribu kuegesha gari pembeni na wao walifanya hivyo hivyo aliamua kwenda moja kwa moja nyumbani na walipofika getini gari moja lilibaki nje na lingine liliingia ndani.”
Ibrahim alisema dereva huyo aliwaeleza kuwa kabla ya watu hao kutekeleza azma yao, Lissu alikuwa tayari kushuka lakini alimzuia licha ya kutaka kushuka kwa nguvu.
“Dereva alisema baada ya kimya kifupi, gari hilo liligeuza tayari kwa kuondoka hapo alishuka mmoja wa watu hao akiwa ameficha uso wake kwa kofia na miwani myeusi, alitoa silaha na kuanza kushambulia gari la Lissu. Dereva alimwinamisha Lissu kwa nguvu kupitia nafasi iliyopo kati ya kiti chake na yeye na alifungua mlango na kujificha chini ya uvungu wa gari nyingine iliyokuwa pembeni,” alisimulia Ibrahim.
Alisema kutokana na hali ambayo alikuwa nayo kijana huyo, walilazimika kumwondoa hospitalini hapo na kumhifadhi.
“Siku ya pili baada ya Lissu kupelekwa Nairobi, dereva wake aliletwa sababu siku ya tukio makamanda wa Chadema Dodoma walimhifadhi na baadaye tulimpeleka Nairobi kupata matibabu ya kisaikolojia kwa kuwa alikuwa mtu wa kwanza kushuhudia damu ya Lissu ikimwagika,” alisema.



'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();