Mechi namba 72 (Mbeya City 0 vs Simba 1).Kamishna wa mechi hiyo Billy Mwilima amepewa Onyo Kali kwa kuruhusu mchezaji Hamisi Msabila wa Mbeya City kucheza mechi bila kuonyesha leseni, hivyo kukiuka Kanuni ya 14(16 na 17) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 81 (Ndanda 1 vs Njombe Mji 1). Klabu ya Ndanda imepigwa faini ya sh 500,000 (laki tano) kwa kutowasilisha orodha ya wachezaji wake (team match list) kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre- match meeting) kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 14(2k) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu dhidi ya Ndanda katika mechi hiyo iliyofanyika Novemba 24, 2017 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.
Pia Kamati imeiomba Sekretarieti ya Bodi ya Ligi kutoa Waraka mwingine kwa klabu kuzikumbusha kuhusu kutoa orodha ya wachezaji kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre-match meeting).
Mechi namba 83 (Yanga 1 vs Tanzania Prisons 1). Tanzania Prisons imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre-match meeting) ikiwa na maofisa watatu badala ya wanne, hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi hiyo iliyochezwa Novemba 25, 2017 Uwanja wa Azam Complex ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.
Wachezaji Lambart Sabiyanka wa Tanzania Prisons na Obrey Chirwa wa Yanga wamesimamishwa kwa kuzingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kutokana na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu, wakisubiri malalamiko dhidi yao kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.