ORODHA YA KWANZA YA MAJINA YA WALIOPATA MIKOPO 2017/2018
Waombaji wa Mwaka wa Kwanza
Tunapenda kuwafahamisha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/2018 kuwa, baada ya uchambuzi wa maombi yao, Orodha ya Awamu ya Kwanza yenye wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza waliofanikiwa kupangiwa mikopo imekamilika.
Kiasi cha Tshs 34.6 bilioni kimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao 10,196 . Kwa ujumla, Tshs 108.8 bilioni zitatolewa kwa wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/2018 .
Orodha hiyo ya kwanza inapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz) na itatumwa kwa vyuo husika. Orodha nyingine (batches) zitafuata kadri taratibu za udahili na uchambuzi zinavyokamilika. Lengo ni kutoa majina ya wote waliofanikiwa kupata mkopo kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba, 2017.
Orodha hii ya wanafunzi 10,196 imepatikana baada ya kupokea na kuchambua Awamu ya Kwanza ya majina ya wanafunzi 32,495 waliopata udahili katika chuo kimoja. Itakumbukwa kuwa moja ya sifa kuu za kupata mkopo ni mwombaji kupata udahili katika taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na Serikali.
Wanafunzi waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja na ambao wana sifa za kupata mikopo, watapangiwa mikopo baada ya kuchagua na kuthibitisha chuo watakachojiunga kwa ajili ya masomo.
Tshs 318 bilioni zatengwa kwa ajili ya wanaoendelea na masomo
Wakati huohuo, tunapenda kuwafahamisha wanafunzi wa elimu ya juu wanaoendelea na masomo na umma kwa ujumla kuwa tunatarajia kuanza kutuma vyuoni fedha za mikopo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wamefaulu mitihani yao kuanzia leo, Jumatano, Oktoba 18, 2017 .
Kiasi cha Tshs 318.6 bilioni kitatolewa kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo kwa mwaka wa masomo 2017/2018. Tayari Serikali imeshatoa fedha hizo na lengo la Bodi ni kuhakikisha fedha zinafika vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ili kuwaondoloea wanafunzi usumbufu.
Hitimisho
Bodi ya Mikopo inawasihi waombaji wa mikopo kuwa na subira wakati ikiendelea kukamilisha maandalizi ya orodha zinazofuata za wanafunzi waliopata mikopo. Tutaendelea kutoa taarifa kwa vyombo vya habari na tovuti ya Bodi mara kwa mara.
Kupata orodha kamili bofya hapa
Mwisho.
Imetolewa na:
ABDUL-RAZAQ BADRU
MKURUGENZI MTENDAJI
JUMATANO, OKTOBA 18, 2017